Leo ni siku ya malaria duniani


Image result for picha za chandaruaWakati ulimwengu ukiadhimisha siku ya malaria leo, shirika la afya duniani WHO limefahamisha hapo jana kuwa chanjo ya kwanza ya ugonjwa huo itaanza kufanyiwa majaribio nchini Kenya, Malawi na Ghana kuanzia mwaka 2018.

Chanjo hiyo ya kiwango kikubwa ilichukua miongo na mamilioni ya Dola kubuniwa.
Mratibu wa mpango wa kutekeleza chanjo hiyo Mary Hamel anasema chanjo hiyo kwa sasa imeshavuka ngazi ya kufanyiwa uchunguzi katika maabara na shirika la kudhibiti dawa la Ulaya limeisifu chanjo hiyo.

Chanjo hiyo iitwayo RTS,S ni kwaajili ya kuwakinga watoto wadogo dhidi ya aina mbaya ya malaria inayosababishwa na mbu aitwae Plasmodium falciparum. Itafanyiwa majaribio katika maeneo yatakayochaguliwa na nchi hizo tatu na maeneo hayo yanatakiwa kuwa na visa vingi vya maradhi ya malaria na pia kampeni za kupambana na ugonjwa huo.

Kulingana na Hamel, chanjo hiyo itatolewa kwa jumla ya watoto 360,000 walio kati ya umri wa miezi mitano na kumi na saba ili kubainisha iwapo dalili za kinga zilizooneshwa katika uchunguzi wa kliniki, zitaonekana pia katika hali ya kawaida ya maisha. Watoto watapokea chanjo hiyo mara tatu kwa mwezi wakiwa na umri wa miezi mitano na watapewa chanjo ya nne watakapotimiza miaka miwili.

Kenya, Ghana na Malawi zina mipango thabiti ya kinga ya malaria
Daktari Edward Mwangi ni afisa mkuu mtendaji wa muungano wa mashirika yasiyo ya kiserikali dhidi ya malaria nchini Kenya KeNaam, na anasema kinga hiyo ni muhimu na itasaidia pakubwa.

"Kwa mfano badala ya mtoto kuwa mgonjwa mara mbili au tatu kwa mwaka kutokana na malaria," alisema Edward, "atakuwa mgonjwa mara moja tu na jambo hili linapunguza idadi pia ya wale wanaokuwa wagonjwa ama wale wanaofariki kutokana na malaria mwisho wa siku," aliongeza afisa huyo wa KeNaam.

WHO inasema Kenya Ghana na Malawi ndizo nchi zilizochaguliwa kwa uchunguzi huo kutokana na kuwa nchi zote hizo zina mipango thabiti ya kinga lakini bado zina visa vingi vya malaria.
Pedro Alonso (picture-alliance/dpa/M. Trezzini)
Mkuu wa kitengo cha malaria WHO Pedro Alonso
Mkuu wa kitengo cha malaria WHO Pedro Alonso
WHO inatazamia kuangamiza malaria ifikiapo mwaka 2040 licha ya changamoto zilizoko katika vidonge na dawa zinazotumika kuwauwa mbu.
Daktari Mwangi lakini anasema kwamba chanjo hiyo haitokuwa mwisho wa malaria barani Afrika na sehemu zilizoathirika na maradhi hayo duniani.
Malaria ni changamoto kubwa ya kiafya inayoikabili dunia
"Chanjo hiyo ni nyongeza tu ya kupambana na malaria na labda kuuangamiza ugonjwa huo barani Afrika na sehemu nyengine," alisema Edward, "kwa hiyo kitakachofanyika ni kuwa, chanjo hiyo itatolewa, lakini zile mbinu zengine zinazotumika ili kujikinga dhidi ya malaria zitakuwa zikitumika pia, kama vile matumizi ya vyandarua na hata unapokuwa mgonjwa utaweza kutibiwa bado," aliongeza mkuu huyo wa KeNaam.


---Chanzo BBC

Popular posts from this blog

RAIS KIKWETE AZINDUA MPANGO WA HUDUMA POPOTE WA BENKI YA POSTA TANZANIA TPB