‘Kwenda Mwanza sasa kwa Sh 32,000 kwa ndege’


Na Gabriel Mushi, Dar es Salaam
WAKAZI wa Mikoa ya Kilimanjaro na Mwanza, wanatarajia kufaidi zaidi usafiri wa anga baada ya Shirika la Ndege la Fastjet kuzindua huduma zake nchini kwa gharama nafuu ya Sh 32,000 kutoka Dar es Salaam kwenda katika mikoa hiyo.

Akizungumza na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam jana wakati wa uzinduzi wa mauzo ya tiketi za safari hizo, Ofisa Mkuu wa Masoko wa shirika hilo, Richard Bodin, alisema wakazi wa mikoa mingine watapata huduma hiyo kila itakapowezekana.

Alisema kwamba, shirika hilo limekuja kuwekeza kwa mara ya kwanza katika Bara la Afrika na kuchagua Jiji la Dar es Salaam ili kukuza masoko na kurahisisha usafiri kwa wakazi wake.
“Uzinduzi huo wa tiketi ni hatua muhimu katika juhudi za kampuni kuwezesha usafiri wa ndege kwa Watanzania kwa sababu wapo wengi ambao awali walikuwa hawamudu gharama za safari za ndege.
“Kwa usafiri wa anga kutoka Dar es Salaam kuelekea Kilimanjaro na Mwanza zitakuwa ni Dola 20 za Marekani sawa na Sh 32,000 kwa wasafiri watakaowahi kwa sababu iwapo wakichelewa baada ya kodi zitapanda hadi kufikia Dola za Marekani 70 hadi 75.
“Fastjet ambayo imeinunua Kampuni ya 540, imechagua Mkoa wa Dar es Salaam kuwa kituo chake cha kwanza cha uendeshaji barani Afrika ambapo safari za ndege zitaanza kuruka kutoka Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere kuanzia Novemba 29 mwaka huu.
“Tiketi za Dar es Salaam kwenda Kilimanjaro na Mwanza zimeanza kuuzwa leo (jana), safari nyingine za ndani na Kanda ya Mashariki mwa Afrika zitaanza baada ya wiki kadhaa.
“Kwa ujumla, hiki ni kipindi cha kihistoria kwa safari za anga Tanzania na hasa Bara la Afrika kwa sababu tumedharimia kuhakikisha usafiri wa anga kwa upande wa bara hili unakuwa ni kitu ambacho kila mtu anaweza kukimudu tofauti na awali,” alisema Bodin.
Kutokana na ujio wa safari hizo, alisema shirika hilo linatarajia kuajiri zaidi ya watumishi 600 ili kukabiliana na tatizo la ajira nchini.
“Lakini pia tumejipanga kukabiliana na soko kwa sababu aina hii ya usafiri wa gharama nafuu tumeuanzia katika nchi za Bara la Ulaya na mpaka sasa unaendelea hivyo tuna uzoefu nao.
“Katika kuhakikisha tunaingia kwenye soko kwa nguvu zote, tunatarajia kuleta ndege tatu aina ya A319 zitakazoanza kutoa huduma mara mbili kwa siku kwa kila mkoa na zitakuwa zikitoa huduma za ubora wa kimataifa,” alisema.

Chanzo: Mtanzania

Popular posts from this blog

RAIS KIKWETE AZINDUA MPANGO WA HUDUMA POPOTE WA BENKI YA POSTA TANZANIA TPB