Rais Jakaya Kikwete Ziara ya Kikazi ya Marekani na Ziara Rasmi ya Kiserikali ya Canada akianzia mjini New York
Rais Jakaya Kikwete |
Rais
wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Jakaya Mrisho Kikwete
anaanza Ziara ya Kikazi ya Marekani na Ziara Rasmi ya Kiserikali ya
Canada akianzia mjini New York, Marekani leo,Jumatatu, Oktoba Mosi,
2012.
Rais
Kikwete na ujumbe wake uliondoka nchini usiku wa jana, Jumapili,
Septemba 30, 2012, na utawasili mjini New York, Marekani mchana wa leo
tayari kwa ziara hiyo ya Marekani. Rais Kikwete atakuwa Marekani kwa
siku mbili kabla ya kwenda Canada kwa ziara Rasmi ya Kiserikali ya siku
mbili.
Katika
ziara yake mjini New York, Marekani, Rais Kikwete atakutana na kufanya
mazungumzo na Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Mheshimiwa Ban Ki Moon
ofisini kwa Katibu Mkuu huyo kesho asubuhi Oktoba 2, 2012.
Baada
ya mazungumzo hayo, Rais Kikwete ataungana na Mheshimiwa Ban Ki Moon,
Meya wa Jiji la New York na Mfadhili Mkubwa wa Misaada yaKibinadamu
Duniani, Mheshimiwa Michael Bloomberg; Mama Helen Agerup ambaye ni
Mwenyekiti wa Taasisi ya Misaada ya Kibinadamu ya H&B Agerup na Dkt.
Kelly J. Henning, Mkurugenzi wa Mipango ya Sekta ya Afya ya Taasisi ya
Bloomberg Philanthropies kwenye Uzinduzi wa Matokeo ya Mpango ya Ubunifu
wa Afya ya Akinamama katika Tanzania.
Kwenye
sherehe hiyo iliyopangwa kufanyika kwenye ukumbi uitwao Green Room
kwenye makao makuu wa Umoja wa Mataifa, Rais Kikwete, Mheshimiwa Ban Ki
Moon, Meya Bloomberg na mama Helen Agerup kwa pamoja watazindua Matokeo
ya Mpango huu uitwao Innovative Maternal Health Program.
Kwenye
shughuli hiyo pia Meya Bloomberg atatangaza matokeo ya miaka mitatu ya
misaada ya kiafya chini ya mpango huo kwa akinamama iliyotolewa na
taasisi ya inayomilikiwa na Meya Bloomberg ya Bloomberg Philanthropies Aidha,
kwenye shughuli hiyo, Meya Bloomberg atatangaza misaada mpya wa
mabilioni ya fedha kuboresha afya ya akinamama katika Tanzania chini ya
mpango huo na atatangaza mshirika mpya ambaye atasaidiana na taasisi ya
Bloomberg Philanthropies katika kuunga mkono huduma bora za afya kwa
akinamama wa Tanzania.
Katika
Tanzania, misaada ya taasisi ya Bloomberg Philanthropies huelekezwa
katika maeneo ya vijijini yasiyokuwa na huduma bora zaidi kwa kiafya na
huduma ambazo hutolewa ni zile za kuokoa maisha ya akina mama hasa
wakati wa uzazi.
Tokea
mwaka 2006, taasisi hiyo imetoa kiasi cha dola za Marekani milioni 11.5
Fedha hizo ni sehemu ya kiasi cha dola za Marekani milioni 330 ambazo
zilitolewa na taasisi hiyo kwa nchi mbali mbali duniani kwa mwaka jana
peke yake.
Taasisi
hiyo hufanya kazi ya kuendeleza maeneo matano duniani ambayo ni Usanii,
Elimu, Mazingira, Ubunifu katika Serikali na Afya ya Umma.
Rais
Kikwete ataondoka Marekani kwenda Canada keshokutwa Jumatano Oktoba 3,
2012 kwa ajili ya Ziara Rasmi ya Kiserikali ya siku mbili katika nchi
hiyo kwa mwaliko wa Gavana Jenerali wa nchi hiyo, Mheshimiwa David
Johnston.
Imetolewa na:
Kurugenzi ya Mawasiliano ya Rais,
Ikulu.
Dar es Salaam.
1 Oktoba, 2012