Chatanda amtunishia misuli Lowassa
Edward Lowassa |
Mara baada ya Msema Chochote (MC) kumpa kipaza sauti Chatanda, alianza kwa kuwatambulisha viongozi hao na kuwapa nafasi ya kusalimia, lakini ilipofika kwa Lowassa alimruka na kumkaribisha Mwenyekiti wa Mkoa aliyemaliza muda wake, Onesmo Nangole ili kumkaribisha mgeni rasmi kufungua mkutano huo.
Kutokana na hali hiyo, wajumbe wa mkutano huo, walianza kupaza sauti huku wakisisitiza ‘bado mjumbe mmoja, bado mjumbe mmoja’ ndipo Chatanda alipomtambulisha Lowassa na kumkaribisha kusalimia wajumbe.
Mara baada ya Lowassa, aliyekuwa kiti cha mbele meza kuu, kusimama ukumbi ulilipuka kwa maneno ya CCM, CCM, CCM ambapo aliwapungia mkono hadi waliponyamaza.
Hata hivyo, Lowassa licha ya kusimama hakusema chochote hadi wajumbe hao waliponyamaza ndipo na yeye akaketi.
Chatanda ambaye anatajwa kuwa katika kambi ya Waziri wa Mambo ya Nje, Benard Membe, amekuwa akilumbana mara kwa mara na wana-CCM ambao wanamuunga mkono Lowassa katika chaguzi mbalimbali.Hata hivyo, baadaye jioni Lowassa alitambulishwa na msimamizi wa uchaguzi huo, Jumanne Maghembe ambaye ni Waziri wa Kilimo, Chakula na Ushirika.
Akizungumza wakati wa kumkaribisha Nangole, Lowassa alisema inawezekana Chatanda alipitiwa kidogo kutokana na hekaheka za chaguzi zilizopita na hasa baada ya watu aliokuwa anawataka kushindwa.
Hata hivyo, Lowassa alimpongeza katibu huyo kwa kazi nzuri alizofanya.
Lowassa amrushia dongo RC
Kwa upande mwingine, Lowassa alimrushia dongo Mkuu wa Mkoa wa Arusha, Magessa Mulongo kuwa ni kijana mdogo, lakini hana shaka naye na akasema kuwa ni mchapakazi na anapaswa kusaidia kutatua matatizo mbalimbali yanayoukabili mkoa huo.
Baadaye jioni mwandishi alimfuata Chatanda na kutaka ufafanuzi kuhusiana na hali hiyo ambapo alijibu kwa mkato kuwa “Sitaki maneno” na kupanda katika gari lake na kuondoka.Hata hivyo, baadaye alimpigia simu mwandishi na kusema, “ Mpaka ifikie mwanaume anitaje, mimi ni jembe na moto ni uleule.”
Awali, katika mkutano huo wa uchaguzi wajumbe wote walimchagua Lowassa kuongoza kikao hicho hatua ambayo ilidhihirisha kuimarika kwa kambi yake mkoani hapo.
Lowassa mara baada ya kuchaguliwa kwa kura nyingi, aliwaeleza wajumbe kuwa amewasikia na hatawaangusha.
Katika uchaguzi huo, mchuano mkali ulikuwa katika nafasi ya uenyekiti, ambapo Nangole ambaye taarifa zinasema yuko kambi ya Lowassa, alikuwa anachuana na Sheikh Adam Chora na Dk Salash Toure.Katika uchaguzi huo, kulikuwa na jumla ya wajumbe 855 kati ya wajumbe 897 ambao walipaswa kushiriki.
Matokeo
Akitangaza matokeo hayo, Maghembe alisema, Ole Nangole ameibuka mshindi wa kiti cha uenyekiti baada ya kupata kura 604 na kufuatiwa na Sheikh Chora ambaye alipata kura 213. Mgombea wa mwisho ambaye ni Dk Toure aliambulia kura 15 ambapo jumla ya wapigakura walikuwa 833 na kura 3 ziliharibika.
MWANANCHI