HAFLA FUPI YA KUWAPONGEZA WAJUMBE WA BUNGE MAALUMU LA KATIBA
Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi akiwa pamoja na Mke wa Waziri Mkuu Mama Tunu Pinda wakijumuika pamoja katika kulisakata rumba kwenye tafrija ya kukaribishwa kwa Wajumbe wa Bunge Maalum la Katiba Mjini Dodoma.
Waziri Mkuu Mh. Mizengo Pinda akiwa na Mke wa Mbunge wa Mpendae Mama Tamima Turky wakionyesha manjonjo yao katika mduara wa tafrija ya kuwakaribisha wabunge wa Bunge Maalum la Katiba wa CCM.
Raha iliyoje kwa Mke wa Waziri Mkuu Mama Tunu Pinda Kushoto, Mke wa Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Mama Asha Suleiman Iddi na Mbunge wa Viti Maalum Chek chake Pemba Mh. Faida Mohd Bakari wakati wakiliskata rumba kwenye tafrija ya kukaribishwa wabunge wa Bunge Maalum la Katiba wa Chama cha Mapinduzi.
Waziri Mkuu wa Serikali ya Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania Mh. Mizengo Pinda akimpongeza Mkurugenzi wa Mlimani Grand Mark Bwana Fredy Sam kwa ubunifu wake wa kujenga Ukumbi wa Kisasa ndani ya Manispaa ya Mji wa Dodoma. Picha na Hassan Issa wa – OMPR – ZNZ.
**********************************
Waziri Mkuu wa Serikali ya Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania Mh. Mizengo Kayanda Piter Pinda amesema majaribio yote ya changamoto zilizotokea ndani ya miaka 50 ya Muungano wa Tanzania lazima yaendelee kulinda na kudumisha amani na utulivu uliopo Nchini.
Mh. Pinda alisema hayo katika tafrija maalum ya kuwakaribisha Wawakilishi wa Baraza la Wawakilishi, Wabunge wa Bunge la Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania pamoja na Wajumbe wa Bunge Maalum ya Katiba wa Chama cha Mapinduzi wanaokutana Mjini Dodoma kujiandaa kujadili Katiba Mpya ya Jamuhuri ya Muungano.
Tafrija hiyo iliyoandaliwa na Ofisi ya Faragha ya Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar kwa kushirikiana na baadhi ya wahisani wakiwemo Wabunge ilifanyika katika Ukumbi wa Kilimani Grand Mark uliopo pembezoni mwa Magharibi ya Mji wa Dodoma.
Waziri Mkuu Mizengo Pinda alisema Dunia imeshuhudia muungano wa Mataifa kadhaa iliyoundwa katika mifumo tofauti hasa ule wa Shirikisho ambayo hatma yake ilikuwa ni fupi na bila ya mafanikio.
Alieleza kwamba waumini na wasimamizi wa Muungano wa Tanzania ambao bado unaendelea kuwa pekee na wa mfano Barani Afrika katika Kipindi cha miaka 50 iliyopita wanapaswa kusimamia Umoja, Mshikamano na Upendo huo uliopo miongoni mwa Wananchi.
Naye kwa upande wake Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi akitoa nasaha zake katika tafrija hiyo alisisitiza kwamba Wabunge wa Bunge Maalum la Katiba ndio watetezi halisi wa Wananchi wote Nchini Tanzania.
Balozi Seif alisema matarajio ya Jamii ya Wananchi wa Tanzania Bara na Zanzibar ni kuendelea kuishi katika maisha ya furaha yaliyojaa matumaini ya kujengeka kwa hatma yao ya baadaye hasa katika kujikwamua kiuchumi.
Alifahamisha kwamba licha ya wananchi walio wengi kutoa maoni yao katika vikao na mikutano ya Tume ya Katiba Mpya ya Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania ya kueleza mfumo wa Katiba wanayoihitaji lakini bado jukumu la kuboresha mfumo huo hivi sasa limo ndani ya mikono ya Waheshimiwa Wabunge wa Bunge hilo Maalum la Katiba.
Alitahadharisha kuepukwa kwa ushabiki na kisiasa miongoni mwa Wabunge hao wa Bunge Maalum la Katiba ambao unaweza kuharibu lengo la Taifa lililokusudiwa la kupatikana kwa Katiba Mpya ya Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania.
Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar aliwapongeza Wabunge wa Bunge hilo Maalum la Katiba kwa kupata fursa hiyo adhimu na kuwaomba kuitumia vyema ili kiu ya Wananachi waliyonayo iwewe kuwafikia.
Mapema Naibu Katibu Mkuu wa Chama cha Mapinduzi Zanzibar Nd. Vuai Ali Vuai alisema uwepo wa Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania ndio uliosababisha Umoja, Upendo na Mshikamano miongoni mwa Wananchi wote wa Tanzania Bara na Zanzi bar.
Nd. Vuai alisema Heshima hii ambayo imekuwa tunu kwa Mataifa mbali mbali Duniani hasa ndani ya Bara la Afrika inafaa kulindwa na kudumishwa kwa faida ya jamii yote.