WAZIRI MKUU MIZENGO PINDA ACHARUKA KASI NDOGO YA UJENZI WA BARABARA RUKWA
TAARIFA KWA VYOMBO VYA HABARI
WAZIRI MKUU Mizengo Pinda jana jioni (Jumamosi, Juni Mosi, 2013) alilazimika kufanya ziara ya ghafla kwenye kambi ya wajenzi wa barabara ya Kanazi-Kizi-Kibaoni ili kupata maelezo ni kwa nini kazi hiyo inasusua na haionyeshi kuendelea.
Waziri Mkuu ambaye alikuwa akitoka Namanyere, wilayani Nkasi, mkoani Rukwa ambako alikuwa mgeni rasmi kwenye uzinduzi wa Maadhimisho ya Siku ya Mazingira Duniani ambayo Kitaifa yanafanyika mkoani Rukwaalilazimika kusimama kwenye kambi hiyo ya wajenzi iliyopo Paramawe, wilayani Nkasi.
Kampuni inayohusika na ujenzi wa barabara hiyo ni China Hunan Construction Engineering Group Corporation (CHCEG) na gharama za mradi huo ni sh. bilioni 82.8/- ambapo hadi sasa kiasi cha sh. bilioni 16.37 kimekwishatolewa na Serikali kwa mkandarasi huyo.
Barabara hiyo ya kutoka Kanazi kupitia Kizi hadi Kibaoni ambayo ina urefu wa km. 76.6, ilianza kujengwa Juni 2009 na ilipaswa kuwa imekamilika Machi 20, mwaka huu lakini hadi sasa haijawekewa hata kilometa moja ya lami.
Ujenzi wa barabara hiyo ni sehemu ya pili ya mradi wa ujenzi wa barabara ya Sumbawanga hadi Mpanda kupitia Namanyere.
Akitoa maelezo mbele ya Waziri Mkuu, Meneja wa TANROADS mkoa wa Rukwa, Mhandisi Florian Kabaka alisema mradi huo uliokuwa umepangwa kukamilika katika kipindi cha miezi 36, unakabiliwa na changamoto nyingi zikiwemo vipindi virefu vya mvua (Desemba – Mei) na kukosekana kwa wataalamu waliobobea kwenye kazi hiyo.
“Awali mradi huu ulikuwa umepangiwa miezi 36 na ulipaswa kuwa umekamilika tangu mwezi Machi lakini kulizuka ubishi wa tarehe ya kuanza mradi na kukawa na tatizo la kukosekana wataalamu wenye sifa zinazostahili pamoja na vipindi virefu vya mvua,” alisema.
Alisema tatizo jingine lililoukumba mradi huo ni mkandarasi kuwa anasimamisha kazi kila mara kwa sababu ya ukosefu wa fedha licha ya kuwa amekuwa akilipwa kwa awamu. “Fedha amekuwa akilipwa kwa awamu lakini alipaswa kutumia hata fedha zake ili kuhakikisha kuwa kazi inakamilika katika muda uliopangwa kwenye mkataba,” alisema Bw. Kabaka.
Alipoulizwa na Waziri Mkuu ni wataalamu gani ambao hawajapatikana, Mhandisi Kabaka aliwataja kuwa ni Meneja Mradi, Mhandisi wa Maabara na Mhandisi wa Barabara.
Naye Mkandarasi wa kampuni ya CHCEG, Bw. David Shi Weiwe alipotakiwa na Waziri Mkuu atoe maelezo juu ya kusuasua kwa mradi huo alisema baada ya kufanya mazungumzo na wakuu wa TANROADS wiki iliyopita huko Dar es Salaam, wameahidi kukamilisha taratibu za kuwapata wataalamu wanaohitajika. Hata hivyo, alisema wanakwamishwa na utaratibu wa upatikanaji wa viza ambao unaweza kuchukua karibu miezi miwili.
Waziri Mkuu alisema miezi miwili ni mingi na akamtaka mkandarasi huyo awasiliane na Mkuu wa Mkoa wa Rukwa, Mhandisi Stella Manyanya endapo kuna vikwazo watakumbana navyo katika kukamilisha kazi yao. Alisema atamwagiza Waziri wa Ujenzi, Dk. John Magufuli akazuru maeneo yote ya ujenzi kuanzia Tunduma hadi Mpanda yakiwemo Sumbawanga na Laela.
Pia alimtaka aongeze kasi ya ujenzi huku akizingatia umakini katika kipindi cha miezi mitano ijayo ambacho hakina mvua ili kukamilisha kilometa 16 za lami ambazo ameahidi mbele ya Waziri Mkuu kwamba zitakuwa tayari ifikapo Novemba, mwaka huu.
Hata hivyo, Waziri Mkuu alimtaka Mkuu huyo wa Mkoa aunde timu ndogo ya watu watano wakiwemo watu wa TANROADS itakayokuwa inafuatilia kazi ya ujenzi wa barabara hiyo pamoja na ile ya Sumbawanga – Matai – Kasanga na kumpa taarifa aiwasilishe kwa Waziri Mkuu kila mwezi juu ya maendeleo ya ujenzi wa barabara hizo mbili.
“Hamuwezi kukaa na kusubiri maamuzi ya kikao cha RCC ambacho ratiba yake ni kukutana mara mbili kwa mwaka. Tumia timu hii ndogo, hakikisha inafuatilia kwa karibu na kutupa taarifa ya nini kinafanyika kila mwezi, nataka tuone katika miezi mitano ijayo tutafikia wapi,” alisema.
IMETOLEWA NA:
OFISI YA WAZIRI MKUU,
JUMAPILI, JUNI 2, 2013.