Mama Kikwete apewa tuzo ya MDGs nchini Marekani


Mke wa Rais na Mwenyekiti wa Taasisi ya Wanawake na Maendeleo, WAMA, Mama Salma Kikwete akipokea tuzo ya Millenium Development Goals, Women Progress Awards,2013, kutoka kwa Ms Jennie Yeung , Rais wa Shirika la Sun Zhong Shan Foundation lililo chini ya United Nations Education, Science, Cultural and Health Advancement  Foundation la nchini Marekani.  Mama Salma alipokea tuzo hiyo baada ya kutimiza baadhi ya malengo ya Millenia katika masuala ya ukimwi, elimu kwa watoto waliokosa fursa  na kuwawezesha wanawake kiuchumi nchini Tanzania. Kulia ni Katibu wa WAMA, Ndugu Daud Nassib na kushoto ni Dr. Judy Kuriansky, Mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Columbia nchini Marekani.


Na Anna Nkinda – New York
Mke wa Rais Mama Salma Kikwete ametunukiwa tuzo ya Malengo ya Maendeleo ya Milinia ya mwaka 2013 kwa wanawake na Shirika la Voices of African Mothers (VAM) la nchini Marekani kutokana na kazi kubwa anayoifanya ya kusaidia jamii wakiwemo wanawake na watoto.

Sherehe ya kukabidhi tuzo hizo zimefanyika  jana katika ukumbi wa mikutano uliopo makao makuu ya  Umoja wa Mataifa  (UN) mjini New York.

Mama Kikwete ambaye pia ni Mwenyekiti wa Taasisi ya Wanawake na Maendeleo (WAMA) amekabidiwa tuzo hiyo kutokana na uongozi wake madhubuti, mafanikio na mchango wake na kujitoa kwake kuwasaidia wanawake na watoto wa Tanzania.

Akikabidhi tuzo hizo Nana – Fosu Randall ambaye ni Rais na mwanzilishi wa shirika hilo alisema kuwa tathimini ilitofanyika  kwa mwaka 2012 juu ya Malengo ya Maendeleo ya Milenia wametambua kwamba malengo matatu yamefikiwa nchini Tanzania   kabla ya muda uliowekwa wa kikomo wa mwaka 2015.

Alisema kuwa wake wa Marais wa Afrika wanamajukumu mbalimbali katika nchi zao ili kufikia Malengo hayo, Taasisi ya VAM imekuwa ikifanya tathimini juu ya hatua zilizofikiwa na Taasisi za wake wa Marais kupitia taarifa za mwaka na zingine zinazowasilishwa.

“Wanawake hawa wanastahili kutuzwa  kwani wamefanya kazi kubwa pamoja na kufanya shughuli zao katika mazingira yenye changamoto nyingi ukilinganisha na wenzao katika nchi zingine.

Hafla ya tuzo hizi siyo tu inasherehekea mafanikio ya wake wa marais wa Afrika bali pia inawahamasisha na kuwatia moyo wakati huu ambapo mwaka 2015 unakaribia”, alisema .

Alimalizia kwa kusema kuwa mara nyingi vyombo vya habari vimekuwa vikiandika habari  zisizokuwa sahihi kutokana na kazi zinazofanywa na wake wa marais lakini vinasahau kuandika mambo mazuri na kazi kubwa wanayoifanya ya kuwasaidia wananchi na kuviomba vyombo hivyo kubadilika na kuthamini kazi kubwa  wanayoifanya.

Akiongea mara baada ya kukabidhiwa tuzo hiyo Mama Kikwete alishukuru kwa tuzo aliyopewa na kusema kuwa Tanzania ni moja ya nchi ambazo zimepiga hatua kubwa sana katika kufikia malengo ya milinia kwani vifo vya watoto vimepungua kwa asilimia 45 na 49 kwa watoto wachanga.

Alisema kuwa haya ni mafanikio makubwa sana japokuwa lengo ni kuondoa kabisa vifo ambavyo vinatokana na sababu ambazo zinazuilika  na katika malengo mengine maambukizi ya Virusi vya Ukimwi (VVU) yanaendelea kupungua kutoka asilimia 5.7 kwa mwaka 2004 hadi asilimia 5.1 kwa mwaka 2011.

Mama Kikwete alisema, “Elimu ya msingi inatolewa bure kwa watoto wote walio na umri unaostahili na hatua kubwa imepigwa katika kupunguza ugonjwa wa maralia na vifo vya akina mama vinavyotokana na tatizo la uzazi”

Kwa upande wa harakati za kumkomboa mtoto wa kike alisema kuwa ni lazima ziendelee na zizingatie changamoto mpya za mazingira mapya kwani unapompatia elimu unampunguzia changamoto za ujinsia na kumpatia huduma ya afya ikiwemo uzazi wa mpango, unamuwezesha kushiriki zaidi shughuli za maendeleo ya kiuchumi, unasaidia familia yake na jamii kuweza kuendelea.
Kwa upande wake Dk. Judy Kuriansky ambaye ni mwakilishi wa Asasi zisizo za Kiserikali zilizo chini ya UN alisema kuwa wake wa marais wanafanya kazi kubwa ya kuisaidia jamii hivyo basi ni jukumu la kila mmoja kuwaunga mkono na kushirikiana kwa pamoja ili kuweza kutimiza malengo ya maendeleo ya milinia.

Dk. Kuriansky alisema kuwa ili kufikia malengo ya milinia inatakiwa kuimarisha miundombinu iliyopo jambo ambalo litasababisha kuifikia jamii kwa ukaribu zaidi na kuweza kutatua changamoto zinazowakabili.

Tuzo hizo zimetolewa kwa mara ya kwanza na shirika hilo kwa kushirikiana na Taasisi ya The reed for Hope (RFHF) na Bethesda Counsel kwa wake wa marais wa Afrika akiwemo Mke wa Rais wa Burundi Mama Dk. Denice Nkurunziza, Mke wa Rais wa Equatorial Guinea Mama Mintou Doucoure  Epse Traore  na Mke wa Rais wa Mali Mama Dk. Malika Issoufou.

Popular posts from this blog

MH. AMANI ABEID KARUME AFUNGUA SKULI YA DONGE ZANZIBAR