Waziri Muhongo akataa chakula hotelini aenda kwa mamalishe

Profesa Muhongo

WAZIRI wa Nishati na Madini, Profesa Sospeter Muhongo amekataa chakula Hoteli ya Mount Meru na kwenda kula chakula cha Mamalishe.
Tukio hilo lililowashangaza watu 13 waliokuwa katika msafara wake lilitokea hivi karibu wakati
Profesa Muhongo alipokwenda Arusha kwenye mkutano wa wataalamu wa umeme wa nchi 11 za Afrika Mashariki, Kati na Kaskazini.
Waziri Muhongo aliandaliwa chakula hotelini hapo, lakini aliwashangaza wenyeji wake ambao ni Shirika la Umeme Tanzania (Tanesco) na uongozi wa wizara yake.
Baada ya kufika katika mgahawa wa Pizza Point uliopo katikati ya mji wa Arusha, Waziri Muhongo aliagiza ugali na samaki kwa bei ya Sh7,000.
Tukio la waziri huyo kukataa kula chakula cha usiku katika hoteli hiyo ya kifahari, iliwashangaza hata wafanyakazi wa mgahawa huo baada ya kupata taarifa hiyo.
Ingawa haikufahamika mara moja sababu za waziri huyo kukataa kula katika hoteli hiyo kutokana na kuchukua uamuzi ghafla, lakini taarifa za ndani zinadai hakutaka kutumia fedha za walipa kodi kwa matumizi binafsi.
“Waziri aliandaliwa chakula katika Hoteli ya Mount Meru Arusha na mpaka tunatoka Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Kilimanjaro (Kia), ilijulikana tunakwenda kwenye hoteli hiyo lakini chakushangaza alipofika karibu na geti la kuingia hapo, akabadili uamuzi na kuamuru apelekwe mahali atakapopata chakula cha Kitanzania, huku akisema haoni sababu ya kula vyakula vya bei mbaya wakati kuna Watanzania hawana umeme,” alisema ofisa mmoja wa wizara hiyo ambaye hakutaka kutajwa na kumkariri Waziri Muhongo:
“Nipelekeni mahali nitakapopata chakula cha Kitanzania, ili tuwe sawa na Watanzania wenye hali ya chini kwani hizi fedha tunazokwenda kula huko ni jasho lao.”  
Hata hivyo, Profesa Muhongo anadaiwa kuruhusu maofisa waliokuwa kwenye msafara wake ambao wangependa kula Mount Meru kuwashusha, ili akitoka kwa mamalishe awapitie kwa sababu kila mtu ana uamuzi wake.
Msafara wa waziri huyo ulikuwa na watu 13 akiwamo Msaidizi wake na Meneja Mawasiliano wa Tanesco, Badra Masoud ambao wote walilazimika kula chakula katika banda la Pizza Point.
Mmiliki wa mgahawa huo, Grace Lyatuu alisema hakutarajia ujio wa waziri huyo na msafara wake, lakini baada ya kutambua kuwa ni Profesa Muhongo akamshukuru Mungu kwa kumfikisha hapo.
“Kwakweli ilikuwa ni usiku mgumu kwangu, kwani msafara ulikuwa mkubwa na wagafla, sikuwa na uhakika wa kupata vyakula vya kuwatosha lakini baada ya chakula kupatikana nikamshukuru Mungu kwani ilikuwa ni usiku na tulikuwa na maandalizi ya kufunga mgahawa,” alisema Lyatuu.
Profesa Muhongo alitumia Sh100,000 kwa chakula cha watu 13 na vinywaji na kuokoa zaidi ya Sh344,500.
MWANANCHI

Popular posts from this blog

RAIS KIKWETE AZINDUA MPANGO WA HUDUMA POPOTE WA BENKI YA POSTA TANZANIA TPB