Vigogo Uhamiaji watiwa mbaroni, Mmoja akutwa na mil 700



Na Upendo Mosha, Moshi
MAOFISA wawili wa ngazi za juu wa Idara ya Uhamiaji Mkoa wa Kilimanjaro, wanashikiliwa na kuhojiwa kwa muda wa saa 12 na Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU), mkoani hapa.

Maofisa hao walikamatwa juzi asubuhi, wakiwa ofisi za uhamiaji Mkoa wa Kilimanjaro na kuhojiwa kwa tuhuma mbalimbali, ikiwamo matumizi mabaya ya ofisi na ubadhirifu wa fedha za umma.

Taarifa kutoka ndani idara hiyo, zinasema maofisa hao wenye cheo cha Naibu Kamishina wa Uhamiaji (DCI), baada ya kukamatwa, walipekuliwa hadi nyumbani kwao.

Akizungumza na MTANZANIA, Ofisa Uhusiano Idara Uhamiaji Mkoa wa Kilimanjaro, Anna Kisaka, alikiri kushikiliwa kwa maofisa na kusema hajui sababu zilizopelekea kukamatwa maofisa hao.

Hatua ya kukamatwa na kuhojiwa kwa viongozi hao, imekuja miezi michache baada ya tume iliyoundwa na Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Dk. Emanuel Nchimbi, kukamilisha uchunguzi wake kuhusu uwepo wa vibali feki.

Habari zinasema, baadhi ya maofisa Uhamiaji katika vituo vya Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Kilimanjaro (KIA), mpaka wa Holili na Moshi mjini, wanadaiwa kuwa na utajiri wa kutisha.

Inadaiwa kuwa mmoja wa maofisa hao, alikutwa na Sh milioni 700 kwenye akaunti yake, huku wengine wakidaiwa kumiliki nyumba na magari lukuki.

Katika hali ya kushangaza, maofisa kadhaa wanaodaiwa kuwa matajiri, walihamishwa kutoka Idara ya Uhamiaji Wilaya ya Hai na kupelekwa mkoani.

Hivi karibuni, Waziri Nchimbi aliunda tume ya watu wanne kutoka makao makuu mjini Dar es Salaam, kwa ajili ya kwenda kufanya uchunguzi wa tuhuma mbalimbali za wafanyakazi wa idara hiyo.

Chanzo: Mtanzania

Popular posts from this blog

RAIS KIKWETE AZINDUA MPANGO WA HUDUMA POPOTE WA BENKI YA POSTA TANZANIA TPB