MABILIONI YA USWISI – TUSIGEUZWE MAZEZETA ;ZITTO KABWE


Jumanne tarehe 20 Novemba 2012, baadhi ya vyombo vya habari vimebeba habari zinazohusu matamshi ya Waziri wa Utawala Bora ndugu George Mkuchika kuhusu sakata ya mabilioni ya Uswisi. Waziri amesema kwamba Serikali ya Uswisi inataka majina ya Watanzania walioficha fedha huko ndio waweze kusaidia uchunguzi. Habari kama Hiyo, yenye maudhui na malengo hayo hayo iliandikwa na Gazeti la The Guardian on Sunday la tarehe 18 Novemba 2012.
Nimeona ni vema nitoe kauli yangu rasmi kuhusu suala hili. Lengo ni kuweka rekodi sawa juu ya Azimio la Bunge na kwamba Serikali inapaswa kutekeleza Azimio na sio kutoa kauli tata za kukata tamaa.
Moja, Suala hili japo sio jipya lakini limeandikwa kama ni jambo jipya. Suala la Serikali ya Uswisi kutaka majina lilisemwa na Mwanasheria Mkuu wa Serikali wakati akichangia hoja binafsi niliyowasilisha Bungeni na pia wakati akileta maombi yake ya kuiondoa hoja ambayo yalikataliwa na Bunge. Kama sio sababu mpya ni kwanini imeibuka upya na kwa kasi? Ni wazi Serikali inajihami kwa kuona kuwa itashindwa kutekeleza azimio la Bunge. Watanzania wasikubali propaganda hii ya Serikali. Bunge limeagiza Serikali kufanya uchunguzi kwa kutumia njia za kiserikali au wachunguzi binafsi wa kimataifa. Kwa nini Serikali inaanza kubwabwaja ilhali wala haijaanza kazi hiyo? Serikali inajaribu kuficha nini? Kwa nini baada ya wiki iliyopita Benki Kuu kufanya uchunguzi kwenye Mabenki ya Biashara jijini Dar es Salaam na namna fedha zimekuwa zikipelekwa nje (international transfers), leo Serikali inakuja na kauli za kukakata tamaa? Kunani?
Pili, Watanzania wajue kwamba Taifa la Swiss limejengwa na linajengwa kwa fedha hizi za wizi ambazo watu mbalimbali duniani wanaiba au kukwepa kodi kwenye nchi zao na kuzificha huko. Serikali ya Swiss hata siku moja haiwezi kutoa ushirikiano kwa Serikali ya Tanzania katika suala kama hili. Ndio maana Azimio la Bunge linataka wachunguzi binafsi ambao hawatahitaji ushirikiano wa Serikali ya Swiss. Nawakumbusha kwamba mwaka 1997 mara baada ya Joseph Desire Mobutu kuangushwa na Rais Joseph Kabila kule Kongo – Kinshasa, Serikali ya Swiss iliitaka Serikali ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo kuonyesha ushahidi kuwa hela hizo za Mobutu zilikuwa zimepatikana kwa njia haramu! Waswiss walitaka Kabila awakakikishie kuwa fedha zile zaidi ya dola bilioni nane za Kimarekani Mobutu hakuzipata kihalali ndio waweze kuzirejesha. Zaire ilikadiriwa kuwa na zaidi ya dola za Kimarekani bilioni thelathini katika Mabenki ya nje ya nchi hiyo. Majibu ya aina aina hii ni majibu ‘standard’ ambayo kila nchi inapewa. Hata Marekani ilipokuwa inafuatilia wakwepa kodi wao walijibiwa hivi hivi. Hatimaye Serikali ya Marekani ikaamua kununua taarifa hizo na kuwakamata wakwepaji kodi wao walioficha fedha Uswisi. Hao ndio Waswiss ambao Serikali ya Tanzania inashabikia majibu yao. Bila Aibu Mawaziri wetu wanayanukuu majibu ya Waswiss kama kasuku. Tunasahau historia haraka sana. Tunakuwa kama mazezeta.
Tusiwe Taifa la mazezeta. Mabwege na mazezeta huimba kila wanachoambiwa kuimba. Sasa Serikali ya Tanzania imekuwa msemaji wa Serikali ya Swiss badala ya kuchunguza utoroshaji wa fedha haramu na kisha kutoa taarifa Bungeni. Naitaka Serikali ianze uchunguzi mara moja kama namna ilivyoelekezwa na Bunge. Suala hili sio suala la kisiasa, sasa ni Azimio la Bunge ambalo linahitaji kutekelezwa kikamilifu. Suala hili sio suala la Zitto Kabwe tena, ni suala la Bunge, ni suala la Wananchi. Wananchi hawataki uzezeta wa watu waliopewa dhamana ya kutekeleza Azimio lao. Kama hawawezi wapishe watu wenye uwezo wa kusimamia maslahi ya Watanzania kwa kuchukua hatua stahili za kuchunguza utoroshaji mkubwa wa fedha za kigeni, ukwepaji mkubwa wa kodi na ufisadi uliopelekea Watanzania kuficha mabilioni kwenye mabenki nje ya Tanzania. Hatutakaa kimya mpaka tuone mwisho kamilifu wa suala hili. Utekelezaji wa Azimio la Bunge itakuwa ni salamu tosha mafisadi na watoroshaji wa fedha haramu kwamba hawana pa kujificha na Tanzania sio Taifa la kuchezeachezea. Lazima tushinde vita hii. Anayeona hawezi kutuongoza kuishinda atupishe mapema. Hatupaswi kuwa Taifa la Mazezeta. Watanzania sio mabwege tena, Mwakyembe alipata kusema.

Kabwe Zuberi Zitto, Mb
Kigoma Kaskazini.

Popular posts from this blog

RAIS KIKWETE AZINDUA MPANGO WA HUDUMA POPOTE WA BENKI YA POSTA TANZANIA TPB