UMOJA WA ULAYA WAWEKA WAZI NIA THABITI YA KUKUZA SEKTA YA NISHATI NCHINI TANZANIA


 Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Mohammed Gharib Bilal, akizungumza na Ujumbe kutoka Umoja wa Mataifa unaoshughulikia Matumizi endelevu ya Nishati kwa wote, wakati ujumbe huo ulipofika Ofisini kwa Makamu wa rais, Ikulu jijini Dar es   Salaam, leo Oktoba 17, 2012 kwa mazungumzo. (Picha na OMR).
Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Mohammed Gharib Bilal, akiwa katika picha ya pamoja na ujumbe wa kutoka Umoja wa Mataifa unaoshughulikia Matumizi endelevu ya Nishati kwa wote, wakati ujumbe huo ulipofika Ofisini kwa Makamu wa rais, Ikulu jijini Dar es   Salaam, leo Oktoba 17, 2012 kwa mazungumzo
Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Mohammed Gharib Bilal, akiagana na (Mshauri wa Nishati Umoja wa Ulaya), Bw. Luis Gomez Echeverri, baada ya mazungumzo yao yaliyofanyika Ikulu jijini Dar es Salaam, leo Oktoba 17, 2012. Kushoto ni Faouzi Bensarsa (Mshauri wa Nishati Umoja wa Ulaya). (Picha na OMR).
Mheshimiwa Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. Mohammed Gharib Bilal leo amekutana na Ujumbe kutoka Umoja wa Mataifa na Umoja wa Ulaya Ikulu jijini Dar es Salaam na kufanya nao mazungumzo ambayo mengi yalijikita katika suala la Nishati Endelevu katika Tanzania.
Ujumbe huo uliwajumuisha;  Bw. Christopher Jones (Mwenyekiti wa Kamisheni ya Maendeleo ya Umoja wa Ulaya), Bw. Faouzi Bensarsa (Mshauri wa Nishati Umoja wa Ulaya), Bw. Luis Gomez Echeverri (Mshauri Mkuu wa Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa, Masuala ya Matumizi Endelevu ya Nishati kwa wote) na Bw. Alberic Kacou (Mwakilishi wa Umoja wa Mataifa nchini Tanzania).
Katika mazungumzo hayo; Bw. Jones alimueleza Mheshimiwa Makamu wa Rais namna Umoja wa Ulaya ulivyo na nia thabiti ya kushirikiana na Tanzania katika kupanga mipango madhubuti itakayowezesha sekta ya nishati nchini kukua na hivyo taifa kuondokana na utegemezi wa nishati hasa ya umeme uliopo sasa. Pia alifafanua kuwa, Umoja huo umeshafanya mazungumzo na Wizara ya Nishati na Madini ya Tanzania na hivyo ni matarajio yake kuwa kupitia ushirikiano baina ya Tanzania na Umoja wa Ulaya, sekta ya Nishati itapata ahueni katika siku zijazo na hivyo kuongeza uwezo pamoja na idadi ya watumiaji wa nishati hasa ya umeme kwa Tanzania.
Kwa upande wake Bw. Bensarsa yeye alimueleza Mheshimiwa Makamu wa Rais kuwa, hii ni mara ya kwanza kwa Umoja wa Mataifa kuweka agenda ya nishati kuwa moja ya agenda zake kubwa na akafafanua kuwa kupitia mpango wa ‘Nishati Endelevu kwa Wote’, Tanzania itaweza kunufaika na fursa zinazotokana na mpango huo na hasa sasa ambapo bado kuna tatizo la nishati japokuwa katika miaka michache ijayo Tanzania inategemewa kuwa na uwezo mkubwa wa kuzalisha nishati ambayo itatumika hapa na nje ya mipaka ya Tanzania.
Mwakilishi huyo wa Umoja wa Mataifa alieleza pia kuwa, Tanzania inakabiliwa na changamoto mbalimbali na moja kubwa ni juu ya kuhakikisha kuwa uzalishaji wa nishati unafanyika kwa kiwango cha juu hali inayoweza kutoa fursa za kukuza uchumi zaidi, pamoja na kuhakikisha inashirikisha wadau mbalimbali wa sekta ya nishati katika kuwekeza kwenye sekta hiyo.
Akizungumza na wageni wake, Mheshimiwa Makamu wa Rais Dkt. Bilal alifafanua kuwa Tanzania imejipanga vema licha ya kwamba inahitaji ushirikiano kutoka kwa mataifa wahisani, makampuni na watu binafsi ili kuwekeza katika uzalishaji wa nishati. Pia akafafanua kuwa, nchi yetu inavyo vyanzo vingi lakini tatizo kubwa lipo katika upatikanaji mtaji wa kuvitumia vyanzo hivyo hasa kile cha Geo-Thermal. Tena Mheshimiwa Makamu wa Rais aliwahakikishia wageni wake kuwa, Tanzania imejipanga kuhakikisha kuwa sekta ya nishati inatanuka na kuondokana na utendaji usioridhisha na kwamba anatarajia kuwepo mabadiliko makubwa ya kiutendaji na kimfumo katika shirika la umeme nchini TANESCO , ili lifanye kazi kwa ufanisi na kuongeza tija kwa watumiaji nishati ya umeme hapa nchini.
Imetolewa na: Ofisi ya Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania
Oktoba 17, 2012

Popular posts from this blog

RAIS KIKWETE AZINDUA MPANGO WA HUDUMA POPOTE WA BENKI YA POSTA TANZANIA TPB