Rais Kikwete ashiriki mazishi ya Waziri Mkuu wa Ethiopa Meles Zenawi









RAIS Jakaya Kikwete jana amejiunga na maelfu ya wananchi wa Ethiopia na viongozi mbalimbali wa Afrika, katika shughuli ya kumzika aliyekuwa Waziri Mkuu wa Ethiopia, Meles Zenawi, aliyeaga dunia Agosti 20, 2012.

Meles aliyefariki dunia akiwa na umri wa miaka 57 amekuwa madarakani kwa miaka 21.

Rais Kikwete aliwasili katika Uwanja wa Meskel Square, katikati ya Jiji la Addis Ababa kwa shughuli ya mazishi iliyochukua kiasi cha saa nne na kuhudhuriwa na maelfu ya Waethiopia na wakuu wa nchi na Serikali 13 za Afrika.

Baada ya shughuli hiyo, mwili wa Zenawi uliokuwa umefikishwa katika uwanja huo kwa maandamano kutoka Kasri la Waziri Mkuu, ulibebwa tena kwa maandamano ya wananchi na askari kwenda katika Kanisa Kuu la Holy Trinity la Madhehebu ya Orthodox, kwa misa na hatimaye kuzikwa katika bustani ya Kanisa hilo.

Maandamano ya kuupeleka mwili wa Zenawi kwenda Meskel Square kutoka nyumbani kwake, yalichukua saa moja na nusu, kupitia mitaa mbalimbali ya Addis Ababa ambayo ilifurika wananchi wenye majonzi na uchungu ya kuondokewa na kiongozi wao.

Katika Uwanja wa Meskel Square, jeneza lililobeba mwili wa Meles liliwekwa katika jukwaa lililoinuliwa katikati ya uwanja na kupambwa kwa bendera ya Taifa la Ethiopia.

Mbali ya Rais Kikwete, baadhi ya viongozi wengine waliohudhuria mazishi hayo ni Rais Mwai Kibaki wa Kenya, Rais Yoweri Museveni wa Uganda, Jenerali Salva Kiir wa Sudan Kusini, Rais Paul Kagame wa Rwanda, Rais Jacob Zuma wa Afrika Kusini na Rais Goodluck Jonathan wa Nigeria.

Wengine ni Rais wa Sudan, Jenerali Omar Hassan El Bashir, Rais wa Somalia, Sheikh Ahmed Sheikh Shariff, Rais Boni Yayi wa Benin ambaye pia ni Mwenyekiti wa Umoja wa Afrika (AU), Rais wa Djibout, Ismail Omar Guelleh na Rais Theodoro Obing Nguema Mbasogo wa Equatorial Guinea.

Miongoni mwa watu waliozungumza katika shughuli ya mazishi alikuwa ni Azeb Mesfin, mjane wa marehemu ambaye alikuwa mpiganaji wa msituni pamoja na mume wake na sasa ni mbunge.

Hotuba ya Mesfin iliwagusa waombolezaji katika shughuli hiyo ya mazishi, kiasi cha baadhi ya wananchi walipiga kelele za uchungu na majozi.

Zenawi aliingia madarakani mwaka 1991 baada ya yeye na wapiganaji wenzake kushinda vita ya msituni dhidi ya Serikali ya Mengistu Hailemariam. 

Nafasi yake ya kwanza ilikuwa Rais akiwa na umri wa miaka 36 kabla ya kuwa Waziri Mkuu wakati Katiba ya nchi hiyo ilipobadilishwa.



Popular posts from this blog

TASWIRA: UZINDUZI RASMI WA KAMPENI ZA CHADEMA KWA UDIWANI WA KATA NNE ZA ARUSHA

RAIS KIKWETE ASAIDIA KUENDESHA HARAMBEE KUCHANGIA WODI YA DHARURA YA WATOTO NA VIFAA VYAKE HOSPITALI YA TAIFA MUHIMBILI