JK azindua Chuo cha Ulinzi cha Taifa



RAIS Jakaya Kikwete, amekiagiza Chuo cha Ulinzi cha Taifa (NDC), kuanza kudahili wanafunzi kutoka nje ya nchi ili kuongeza wigo wa utendaji, ikiwa ni pamoja na kupata fikra zaidi katika masuala ya ulinzi na usalama wa taifa.

Rais Kikwete alitoa wito huo jijini Dar es Salaam jana, wakati akizindua rasmi chuo hicho ambacho ni cha kwanza kujengwa nchini.

Alisema kwamba, kukamilika kwa chuo hicho, kutapunguza gharama na kuongeza wigo kwa viongozi wengi zaidi wa Serikali kupata mafunzo ya ulinzi na usalama kwa Watanzania.

“Ndoto ya Watanzania sasa imetimia, kwa sababu tangu mwaka 1964 lilipoanzishwa Jeshi la Ulinzi, hakukuwa na chuo cha aina hii, viongozi wa juu wa jeshi walikuwa wakipelekwa katika vyuo vya Kenya na India kwa ajili ya mafunzo ya kijeshi.

“Lakini pia, kwa kuwa chuo hiki kitatoa mafunzo tofauti na yale yanayotolewa katika vyuo vingine, tunatarajia kupata viongozi wenye kufuata maadili zaidi katika utendaji wao.

“Vyuo vingine vya kijeshi vilivyopo hufundisha zaidi mafunzo ya kupigana, lakini chuo hiki ni tofauti kwa sababu kitakuwa kinatoa mafunzo ya masuala ya ulinzi na usalama wa taifa kwa kuzingatia maadili.

“Kutokana na umuhimu wa chuo hiki, nawasihi mkitunze sana kama methali isemayo, ‘Kitunze Kidumu’, kwa sababu tunatarajia kuvuna viongozi waliosheheni maadili na wenye uwezo wa kutunga sera kwa maslahi ya taifa letu,” alisema Rais Kikwete.

Naye Mkuu wa chuo hicho, Meja Jenerali, Charles Makakala, alisema hadi sasa chuo hicho kimedahili wanafunzi 20 kutoka katika taasisi mbalimbali za Serikali.

“Nane wametoka jeshini, wawili Jeshi la Polisi Zanzibar, Ofisi ya Rais Zanzibar na wengine waliobakia ni katika taasisi mbalimbali, kama vile Wizara ya Nishati na Madini, Wizara ya Mambo ya Ndani na taasisi nyingine.

“Mafunzo yatakuwa ya muda wa wiki 47 kwa kuhusisha programu nne kwa mwaka na tunatarajia kupata wakufunzi kutoka katika vyuo mbalimbali, kama vile UDSM na Chuo cha Diplomasia,” alisema Makakala.

Mtanzania

Rais Jakaya Mrisho  Kikwete akikata utepe kufungua rasmi Chuo cha UIinzi (National Defence College) Septemba 10, 2012 Kunduchi jijini Dar es salaam. Kulia kwake  ni  Mkuu wa Majeshi ya Ulinzi Jenerali Davis Mwamunyange na kushoto kwake ni Mkuu wa Chuo hicho, Meja Jenerali Charles Makalala na kushoto kabisa ni Balozi wa China nchini Tanzania Mhe. Lu Younqing.

Rais Jakaya Mrisho Kikwete akipeana mikono na Mkuu wa Chuo cha UIinzi (National Defence College) Meja Jenerali Charles Makalala Septemba 10, 2012  baada ya kumkabidhi mfano wa funguo kama ishara ya kufungua rasmi chuo hicho kilichopo   Kunduchi jijini Dar es salaam. Kulia  ni  Mkuu wa Majeshi ya Ulinzi Jenerali Davis Mwamunyange.

Rais Jakaya Mrisho Kikwete akiwa na Mkuu wa Chuo cha UIinzi (National Defence College) Meja Jenerali Charles Makalala  baada ya kufungua rasmi chuo hicho kilichopo Kunduchi jijini Dar es salaam. Nyuma yao ni Waziri wa Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa Mhe Shamsi Vuai Nahodha anayefuatana na  Mkuu wa Majeshi ya Ulinzi Jenerali Davis Mwamunyange.

Popular posts from this blog

RAIS KIKWETE AZINDUA MPANGO WA HUDUMA POPOTE WA BENKI YA POSTA TANZANIA TPB