Dk Mwakyembe awapa polisi siku 14 kuwataja polisi wa mafuta

Dk Harrison Mwakyembe
WAZIRI wa Uchukuzi Dk Harrison Mwakyembe, amewashukia polisi nchini kwa kuendelea kufubia macho vitendo vya uhalifu na kuahidi kuchukua mkondo mpya kukabiliana na vitendo hivyo.

Akizungumza katika ibada maalumu ya shukrani iliyofanyika mwishoni mwa wiki katika Kanisa la Nduli lililopo Ikolo, Kijiji alichozaliwa, Dk Mwakyembe alimtaka Kamanda wa Kanda Maalumu Dar es salaam, kuyaweka wazi majina ya askari wote walioshiriki katika wizi wa mafuta bandarini vinginevyo atahakikisha sakata hilo linakwenda mbali zaidi.

Dk Mwakyembe ambaye alitumia muda mwingi kuelezea matukio aliyokumbana nayo kuanzia mwaka 2009, alitoa muda wa wiki mbili kwa polisi kuwataja askari waliohusika na wizi huo vinginevyo alitishia kulifikisha katika ngazi za juu ili wahusika wake wachukuliwe hatua.

“Kamanda Kova ana muda wa wiki mbili kushughulikia suala hilo, kabla ya mimi kulifikisha suala hilo ngazi nyingine ili askari hao waweze kuchukuliwa hatua za kisheria badala ya kuendelea kuwakumbatia askari wasio waadilifu na wanawachafua polisi wema”,alisema Dk Mwakyembe.

Kuhusu misukosuko aliyokumbana nayo pamoja na ugonjwa wa ajabu uliopata hivi karibuni, Dk Mwakyembe alisimulia mlolongo wa matukio kadhaa likiwamo la ajali aliyoipata mkoani Iringa wakati akiwa safarini.
“Mwaka 2009 nilipata ajali mbaya kati ya Makambako na Iringa mjini, kitu ambacho sitokisahau milele ni kwamba niligongwa na lori,” alisimulia.

Alisema pamoja na tukio hilo na matukio mengi mengine yaliyomwandama na kuyaripoti polisi, lakini amekuwa akishangazwa na watendaji wa polisi  kwa kuyasemea matukio hayo pasipo kuyafanyia uchunguzi jambo ambalo limekuwa likimkera na kupoteza imani.

Alisimulia  mikasa inayomwandama alikisema aliandaliwa mpango wa kuuawa kati ya Iringa na Mbeya na aliyepangwa kumuua ni mhalifu sugu, lakini Mungu alijiinua. Muuaji alimfuata akamwambia unaenda safari ya Kyela, usiende, ukienda nitakua,” alisimulia Dk Mwakyembe akiacha watu wamepigwa butwaa.
Alisema ajali ilikuwa mbaya na ilipangwa na kwamba lakini cha ajabu hata polisi waliofika eneo la tukio walikata tama ya kunipeleka hospitali.

Alisema aliokolewa na kwa mujiza ya Mungu kwani aliojitokeza Mkurugenzi wa shule za sekondari na vyuo katika Mikoa ya Nyanda za Juu Kusini, Mboka Mwambusi, ndiye alilazimisha ampeleke hospitali.

 “Aliyenichukua pale alinieleza kwamba polisi aliyemkuta alisema Dk Mwakyembe alikuwa amefariki  dunia  lakini yeye alinisisitizia kuwa kunipeleka hospitali”alisema.

Akifafanua kuhusu vitisho vya kuawa alisema muuaji huyo alimweleza mpango mzima wa mauaji ulivyopangwa na kumpa uhuru wa kumrekodi maelezo yake, ambayo ameyahifadhi hadi leo.

Alisema katika matukio yote yaliyomsibu ndani ya miaka mitatu, Dk Mwakyembe alikuwa akiwaarifu polisi, lakini  hawakuchukua hatua zozote zaidi ya kuendesha juhudi za kuficha ukweli.

Kuhusu ugonjwa wake alisema nayo ni utata mtupu kwani katika mazingira ya kushangaza kumekuwapo na juhudi za kuupotosha umma.

“Mwaka 2011 niliugua, cha kusikitisha niliugua wakati huohuo na kaka yangu, Profesa Mark Mwandosya, Mungu ni mwema, alitunyanyua vitandani, leo tunatembea, mimi na kaka yangu Mwandosya ni ushahidi juu ya utukufu wa Mungu,” alisema Dk Mwakyembe.

“Daktari aliyenitibu aliniambia, amefanya kazi hiyo kwa zaidi ya miaka 27, hakuwahi kuona ugonjwa wa aina ile,” alisema Dk Mwakyembe.

“Sitta alipofika kuniona, nilisikitika sana kwa nini alikuja, ndio maana aliporudi alikuja na kilio kwa polisi akiwataka wachunguze, wakamgeuzia kibao, walisau kuwa Sitta ni Mwanasheria aliyebobe.”

Katika ushuhuda wake, Waziri wa Afrika Mashariki, Samwel Sitta, alihitimisha kwa kuhoji  “Mungu hapendi uongo, na ukweli hauna tabia ya kujificha, ipo siku utadhihirika, ikiwa polisi walikuwa  wanachunguza ugonjwa uliomsibu Dk Mwakyembe, kwa nini hawakwenda kwenye hospitali aliyokuwa akitibiwa?” alihoji.



MWANANCHI

Popular posts from this blog

RAIS KIKWETE AZINDUA MPANGO WA HUDUMA POPOTE WA BENKI YA POSTA TANZANIA TPB