RAIS KIKWETE AONANA NA RAIS MPYA WA GHANA, ATEMBELEA MASHAMBA YA MANANASI
Rais Jakaya Kikwete, amesema Tanzania itatuma wataalamu wa kilimo na wakulima wa zao la nanasi nchini, kwenda Ghana kujifunza ukulima wa kilimo cha kisasa cha aina mpya ya nanasi ambayo ndiyo yenye soko duniani.
Rais Kikwete aliyasema juzi, wakati alipotembelea mashamba mawili makubwa ya kilimo cha kisasa cha mananasi aina ya MD-2, ambayo ndiyo inauzwa zaidi duniani, katika siku yake ya tatu ya ziara ya siku nne nchini Ghana.
Rais Kikwete, aliamua kutembelea mashamba hayo ya Koranco Farms katika Kijiji cha Obotweri na lile la Bomart Farms, lililoko Kijiji cha Dobro, eneo la Nsawan, yote mawili yakiwa kiasi cha kilomita 150 kutoka mjini Accra, ili kujionea mwenyewe kilimo cha aina mpya ya mananasi iitwayo MD-2, ambayo iliingizwa Ghana kutoka nchi ya Costa Rica, kiasi cha miaka 30 iliyopita.
Mananasi aina ya MD-2 , ndiyo yanayouzwa duniani na mbegu aina hiyo ya mananasi haipo Tanzania, ambayo wakulima wake, wanaendelea kulima na kupanda aina ya asili ya mananasi ambayo hayana soko duniani.
Ziara hiyo, Rais Kikwete ambaye alisindikizwa na Waziri wa Chakula na Kilimo wa Ghana, Kwesi Ahwoi ilianzia shamba la Koranco Farms ambalo lilikuwa shamba la kwanza Ghana kulima mananasi aina ya MD-2.
Kwenye shamba hilo, Rais Kikwete ameambiwa kuwa yeye ni Rais wa pili wa Tanzania kutembelea shamba hilo, kufuatia ziara ya Baba wa Taifa, Mwalimu Julius Nyerere, wakati wa ziara yake Ghana miaka ya 1980.
Kwenye shamba hilo, lililoanzishwa miaka 30 iliyopita na lenye ukumbwa wa ekari 800, Rais alitembelea shamba lenyewe na kiwanda ambacho vyote vinakadiriwa kuwa na thamani ya dola za Kimarekani milioni 20.
Mkurugenzi Mtendaji wa shamba hilo, Emmanuel Koranteng amemweleza Rais Kikwete kuwa, shamba hilo linaajiri wafanyakazi 50, inapandwa kiasi cha miche 60,000 katika eka moja na mananasi yake yanauzwa katika nchi wanachama wa Umoja wa Ulaya (EU).
Kwenye shamba la Bomarts, Rais Kikwete ameelezwa na Mtendaji Mkuu wa shamba hilo, Anthony Botchway kuwa, shamba hili lilianzishwa miaka 27 iliyopita na kuwa mananasi aina ya MD-2 yamekuwa maarufu zaidi kuliko aina nyingine duniani.
Amesema kuwa nchi ya Costa Rica inajipatia pato la kiasi cha dola za Marekani milioni 600, kwa kusafirisha na kuuza mananasi aina hiyo nje ya nchi hiyo.
Rais Kikwete ambaye alikuwa katika ziara ya siku nne nchini Ghana, ambako pia ameshiriki mazishi ya aliyekuwa Rais wa nchi hiyo, Hayati John Evans Atta Mills, anaondoka huko kesho kurejea nyumbani.